HAKUNA kitu kibaya maishani kama kuonekana upo katika daraja la chini
na mtu wa kudharaulika kwenye jamii unayoishi. Kisaikolojia kuna
madhara makubwa.
Ni imani yangu kuwa kila mwanadamu timamu anapenda kuheshimiwa lakini
wengi wetu tunashindwa kupata heshima tunayoitaka kwa sababu hatufahamu
jinsi ya kuishi mbele ya wenzetu.
Kitaalamu, hakuna jambo ambalo
hutokea maishani bila sababu maalumu hivyo hata kudharauliwa kwako au
kwetu ndani ya jamii tunayoishi kunatokana na jinsi tunavyoenenda.
Mwalimu
wangu wa somo la maisha na saikolojia, Eric Shigongo, aliwahi kuniambia
‘Nothing happens in the sky, but the elements should be there,’
akimaanisha kuwa hakuna kitokeacho angani pasipo kuwa na dalili au
sababu zake.
Naomba nianze kutoa njia za kukusaidia kurejesha heshima
yako kwa kuperuzi na wewe baadhi ya dokezo muhimu zinazoweza kukusaidia
kujitambua na kuweza kuyaepuka maisha ya kudharauliwa.
MUONEKANO
Kwanza kabisa ni jinsi unavyoonekana. Muonekano
ninaouzungumzia hapa ni usafi wa mavazi na mwili kwa ujumla. Hata siku
moja hakuna mchafu anayeheshimika katika jamii anayoishi hata kama ana
kipaji kikubwa kiasi gani.
Kwa hiyo uchafu wa mavazi na mwili
huchangia mtu kudharauliwa katika jamii anayoishi. Linaweza kuwa jambo
dogo sana lakini ni moja kati ya sababu kubwa inayochangia kuporomoka
kwa thamani yako mbele ya wenzako.
MAZUNGUMZO
Hapa naomba nieleweke kuwa unachokizungumza kinaweza
kukujengea heshima au kukubomolea heshima. Kauli zisizo na busara
zitakufanya udharaulike kwa kila mtu. Uropokaji usiokuwa na mantiki
huchangia kuporomosha heshima yako hasa kama utakuwa muongeaji zaidi.
Biblia inasema penye wingi wa maneno hapakosi uovu.
UTENDAKAZI WAKO
Ndugu zangu, siku zote heshima ya mtu ni kazi.
Watu wengi hawapendi kufanya kazi kwa bidii huku wengine wakijiendekeza
kwa tabia ya kuombaomba, jambo hilo halifai kwa vile huchangia kubomoa
heshima yako mbele ya jamii. Fanya kazi usiishi bila kujishughulisha.
KUTOTIMIZA AHADI
Kama una tabia za kuahidi mambo halafu unashindwa
kuyatekeleza, basi unajiweka katika nafasi mbaya ya kutunza heshima
yako katika jamii unayoishi. Bora ukwepe kutoa ahadi kuliko kuahidi na
kutotimiza.
SIFA ZISIZO NA MAANA
Nakumbuka msemo mmoja kutoka kwa mwandishi
mwandamizi aliyekuwa mtaalamu wa falsafa za maisha, marehemu Adolf
Balingilaki, ambao unasema kwamba:
“Ukitafuta heshima kwa gharama ya juu, basi utalipwa dharau kwa bei nafuu.”
Msemo
huu unamaanisha nini? Siku zote ukiwa unafanya mambo yako kwa ajili ya
kusifiwa au mazungumzo yako kuwa ya kujiinua, watu watakudharau.
KUTOKUWA MWAMINIFU
Suala
la uaminifu ni pana, kuna uaminifu wa fedha, siri, dhamana na mambo
kama hayo, hivyo ni vema kila unachoaminiwa lazima ukitunze kwani ukiwa
mtu wa kuvunja uaminifu fahamu kuwa utashusha heshima yako.
No comments:
Post a Comment