TUANZE kwa kutafakari baadhi ya taarifa za kuhuzunisha, ambazo wengi
wetu tunakutana nazo kila siku katika maisha yetu. “Kuanzia leo
umefukuzwa kazi”, “Nimeamua tuachane”, “Baba yako mzazi amefariki leo
asubuhi”, “Mwanao amefariki.” Bila shaka taarifa za aina hii
zinahuzunisha na swali linabaki tufanyeje tunapokuwa na mawazo ya aina
hii?
Ukweli ni kwamba, yakitokea mawazo mabaya katikati ya furaha
huwezi kuiondoa, lakini pamoja na hayo baadhi ya watu hutumia muda
mwingi sana kuhuzunishwa na tatizo ambalo pengine lingeweza kumalizwa
kwa saa chache na mhusika kubaki huru.
Wapo watu kati yetu
wanaweza kufuga mawazo ya kuachwa na wapenzi wao kwa miaka mitano
mfululizo, huku wengine wakitumia miezi mingi kuondokana na huzuni
iliyotokana na kutukanwa na wazazi, kufokewa na bosi, kupata hasara
katika biashara, kufeli mitihani na kadhalika.
Hii ina maana
kuwa ni wachache kati yetu tunaofahamu namna ya kupambana na mawazo
yanayohuzunisha na kuyashinda. Kwa kuzingatia umuhimu wa kutunza furaha
yetu katika maisha, nimeona ni vema nikawafundisha hatua za kuondokana
na mawazo yanayoumiza yatokanayo na matukio ya kuhuzunisha.
KWANZA:
Mtu anapojikuta katika mawazo ya kuhuzunisha lazima, aanze kwa
kurekebisha kwanza mhemko wake kwa kushughulikia mfumo wa upumuaji.
Unapoletewa taarifa mbaya, moyo hushtuka na kuufanya uende mbio, hivyo
ili kuurudisha katika hali yake ya kawaida unatakiwa kuvuta pumzi kwa
wingi ndani na kuzitoa nje pole pole. Hatua hii itasaidia kurudisha
mapigo ya moyo katika hali yake ya kawaida.
PILI: Baada ya zoezi
hilo, mwenye mawazo ya kuumiza anatakiwa kujilazimisha kutabasamu mara
kwa mara, hata kama hawezi kufanya hivyo kwa wakati huo kutokana na
tukio lililomletea mawazo mabaya. Kutabasamu husaidia kuchangamsha
akili, ingawa inaweza kuchukua muda kurudi katika hali ya kawaida,
lakini wataalamu wanasema inasaidia kuamsha hisia za furaha zilizokuwa
zimeshambuliwa na mawazo mabaya.
TATU: Katika hali ya kawaida
uvamizi wa mawazo mabaya unapotokea hukuta mawazo mengine yakiwemo
akilini na kuyaondoa, kisha yenyewe kuchukua hatua za kutawala akili,
unashauriwa baada ya kutekwa na mawazo hayo chukua hatua ya
kujilazimisha kurudisha akilini mawazo yaliyokuwemo awali kabla
hujavamiwa. Lengo ni kutafuta nafuu na kufufua mawazo yenye kufurahisha.
NNE: Ikiwa wewe mwenyewe huwezi kufurahi baada ya kuchukua hatua hizo, wasaidie wengine waliopo karibu yako kufurahi.
Kwa
mfano unapokuwa kwenye msiba unalia, chukua jukumu la kuwanyamazisha
wenzako na kuwapa faraja. “Nyamazeni, kazi ya Mungu haina makosa”
ukifanya hivyo utakuwa umejisaidia wewe pia kuondokana na mawazo ya
msiba yaliyokufanya ulie sana.
No comments:
Post a Comment